Siku ya UKIMWI 1 Disemba 2019-Mkoani Mwanza, Tanzania

Hadi sasa Watanzania milioni.1.4 wanaoishi na VVU ambapo kiwango cha maambukizi kikiwa ni asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 7.0 ya mwaka 2014.Hayo yamesemwa leo na Mgeni rasmi wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya UKIMWI duniani na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemevu Mhe. Jenista Mhagama jijini hapa. Waziri Mhagama amesema kuwa maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na UKIMWI pia yamepungua.

“Tumeweza kupata mafanikio haya kufuatia kuboreshwa kwa huduma.za ART na afua za kinga kama vile utahiri wa kitabibu wa wanaume na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”, alisema Waziri Mhagama.Aidha, amesema kiwango cha watu wanaoishi na VVU walioko kwenye mpango wa ARV kimeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 57 ya mwaka 2017.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema mpaka kufikia mwezi Septemba 2019 takribani watu 1,252,205 kati ya wananchi 1,600,000 wanaokadiriwa kuishi na VVU nchini walikuwa wamepima na kufahamu hali zao za maambukizi ya VVU.”Hii ni sawa na asilimia 78.3 ya lengo la 90 ya kwanza. Miongoni mwao wanaume walikuwa 413,985 sawa na asilimia 33, na wanawake walikuwa 838,220 sawa na asilimia 77″.alisema. Kwa upande wa vijana Waziri Ummy amesema kuwa Vijana balehe (umri wa miaka 10 – 19) walikuwa 57,167 sawa na asilimia 4.6, na vijana (umri wa miaka 15 – 24) walikuwa 96,006 sawa na asilimia 7.7. Aidha, amesema kati ya waliopima na kutambua afya zao watu 1,221,799 sawa na asilimia 97.6 wanatumia ARV. Hata hivyo alisema Lengo la 90 ya pili ambalo ni asilimia ya kuwa watu waliopimwa na kugundulika kuwa wana maambukizi ya VVU wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU (yaani ARV’s), tayari tumefikia takriban asilimia 98 wanatumia zawa za kupunguza makali ya VVU yaani ARV. “Lengo la 90 ya tatu, ambalo ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya wanaotumia ARV’s wamefanikiwa kupunguza wingi wa VVU mwilini Waziri huyo alisema wamefanya vizuri sana,”ni kuwa tumekuwa tukifuatilia kwa karibu hali za watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU”.Alisema.